Recent Posts
▼
Makongo sekondari
MTULIA AWAPONGEZA SEKONDARI MAKONGO KUJITOLEA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA MWANANYAMALA
MBUNGE wa Kinondoni, Abdallah Mtulia ameupongeza uongozi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makongo inayosimamiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kujitolea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika kumuenzi Mwal. Nyerere Shule hiyo imepaka rangi jengo la wodi ya watoto na kuipatia katoni 100 za maji kwa ajili ya kutumika na watumishi wanaofanya kazi ndani ya wodi maalum ya watoto wachanga (njiti), hospitali hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Daniel Chongolo, Mbunge Mtulia, amesema pamoja na hayo, katika kumuenzi Mwal. Nyerere, Shule hiyo pia wamefanya usafi wa mazingira, wamepanda miti na maua na kuchangia damu.
“Tunafanya yote haya kumuenzi Mwalimu Nyerere, alituhimiza upendo, umoja, uzalendo na kusaidiana, na akatuletea sera ya ujamaa na kujitegemea.
“Huu ni mfano wa kuigwa, tuendelee kumuenzi kwa kufanya yale aliyotuagiza, mengi mazuri, alifanya mambo enzi za uhai wake, alijenga viwanda vidogo na vya kati na hospitali mbalimbali ikiwamo hii ya Mwananyamala.
“Alitutengenezea Majeshi madhubuti mfano hili la JWTZ tangu 1964 alipolianzisha limekuwa nguzo muhimu kwetu, tunaheshimika hata majirani (nchi zingine),wanatujali na tupo salama kwa sababu Jeshi letu lipo madhubuti,” amesema.
Akizungumza, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Makongo, Kanali Yuda Kitinya, amesema “Tumefanya hivi lengo letu hasa ni kuwafundisha vijana wetu uzalendo, wafahamu kwamba wana jukumu la kujitoa kwa ajili ya jamii inayowazunguka, tumechanga fedha kiasi sisi wenyewe na kufanya yote hayo.
“Naamini wataendelea kujitolea kwa jamii, sisi ni chachu tu, kama chumvi kwenye jamii.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Isdory Kiwale, ameshukuru kwa mchango ambao umetolewa na Shule hiyo.
“Tunashukuru sana, huu ni mchango mkubwa kwetu, kujitolea damu ni uzalendo, nawasihi watanzania wengine nao waige mfano huu mzuri, wajitolee, kuchangia damu kwani inahitajika ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji,” amesema Dkt. Kiwale.